Imefasiriwa na Ummu Ahmad
MANUFAA YA NDOA
1. Kupata kizazi ambacho kwanza kitasaidia katika ujengaji wa jamii, pili kueneza jinsia ya watu wa kila kabila au mataifa mbali mbali, na kubwa zaidi ni kuongeza idadi ya kizazi cha jamii ya kiislamu.
2. Kumridhisha Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa kueneza idadi ya wafuasi wa dini ya Kiislamu.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika hadithi sahihi:
“Oeni wake wema muwapendao na wataowapatia kizazi chema, kwani siku ya Kiyama nitajivunia ukubwa wa umati wangu.” [Imam Ahmad]
3. Kupata baraka za mtoto mwema ambaye atakayemsomea dua mzee wake (atakapofariki). Maneno haya yamethibitishwa na hadithi maarufu inayosema kuwa:
“Binaadamu anapokufa, basi amali zake nzuri hukatika au humalizika, isipokuwa mambo matatu makuu nayo ni: Sadaka yenye kuendelea, Elimu yenye kunufaisha na Mtoto mwema atakayemuombea dua mzee/wazee wake.” [Riyadhus-Swaalihiyn]
Faida nyenginezo zipatikanazo katika ndoa ni:
4. Kinga kutokana na shetani katika mambo yanayopelekea au yanokaribisha tendo la zinaa.
5. Utulivu wa akili na moyo na kuwa na urafiki ambao hupelekea mapenzi na huruma baina ya mume na mke.
6. Kunganisha kwa Familia za pande mbili za uukeni na uumeni.
7. Kusaidiana katika kazi za nyumba (sio kumuachia mke kazi zote za ndani ya nyumba). Hii ni tabia ambayo ingalipo kwa baadhi ya akina baba. Kwa vile tabia hii imekuzwa na utamuduni wetu wa tunakotoka, kinyume kabisa na maamrisho ya dini yetu ya kiislamu yanavyotuagiza.
8. Kuelimishana majukumu ya kifamilia. Pia kuweka bidii na kuwa tayari kuihami na kuitunza familia. Na vile vile kuishughulikia na kuitimizia mahitaji yake yakiwa ama ya (kimwili, kimavazi, kisiha, kimawazo na kiroho) na kustahamiliana pale panapotokea kutoelewana.
MATATIZO KATIKA NDOA
Wakati huo huo kuna matatizo yanayopatikana katika ndoa ambayo inabidi tuzingatie na kujichunga ili tuepukane na matatizo hayo. Nayo ni kama yafuatayo:
1. Kushindwa kuchuma pato la halali, ambapo itapelekea kutafuta njia ambazo si za halali za kimapato ili kuweza kutimiza mahitaji ya familia. Haimfalii mke kumlazimisha mumewe ampatie mambo yaliyo nje ya uwezo wa mume. Na tuwaige wanawake wema waliopita, ambao kila waume zao wakitoka kwenda kwenye shughuli zao za kutafuta riziki, wakiwausia kuwa wasirejee na chochote cha haramu. Wakiwanasihi waume zao kuwa ni bora wastahamili kwa njaa ya hapa duniani kwani adhabu ya kesho akhera sio ya kustahamilika.
2. Kushindwa kutimiza majukumu ya ndoa, na hasa kutimiza haki za mke au kutoweza kustahamili kwenye wakati mgumu wa kimaisha. Na tuwe makini katika suala hili kwani kuna ile dhana ya kuwa ndoa ni jambo la kujionyesha tu kuwa fulani kaoa au kaolewa.
“Kila mmoja kati yenu ni mchungaji, na kila mmoja kati yenu atapaswa kuulizwa ya juu ya kile anachokichunga. Mume ni mchungaji wa familia yake, naye atapaswa kuulizwa juu ya anaowachunga. Na mke ni mchungaji wa nyumba ya mumewe, naye pia atapaswa kuulizwa juu ya anachokichunga. Hivyo basi, kila mmoja kati yenu ni mchungaji ambaye atapaswa kuulizwa juu ya anaowachunga” (Bukhari, Muslim)
3. Kuacha kushughulikia mambo muhimu ya kidini, kwa mfano kutumia muda mwingi katika mambo ya anasa za kidunia kama vile kuangalia Televisheni, kwenda kwenye shehere za kuzaliwa mtoto au kwa kutimiza umri fulani wa mtoto (birthday na party), badala ya kutumia muda huo kwa kutengeneza maisha ya akhera ambayo ndio ya milele. Kama tunavyotanabahishwa kwenye Quraan Tukufu Sura ya sitini na tatu aya ya tisa.
((Enyi mlioamini! Yasikusahaulisheni mali yenu, wala watoto wenu, kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndio walio katika khasara))
[Al-Munaafiquun:63:9]
Mtunzi wa mada hii amemalizia kwa kusema kuwa:
Dinar unayoitumia katika njia za Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu Wa Ta'ala), Dinar unayoitumia kumuachia huru mtumwa, Dinar unayoitumia katika kutoa sadaka kwa mtu anayehitaji sadaka hiyo, basi hakuna Dinar iliyo bora kati ya dinar hizo ila ile unayoitumia kwa ajili ya familia yako.
Msemo huu una maana ya kwamba hakuna jambo muhimu katika mafundisho ya kijamii ya kiislamu kama lile la kuzishughulikia familia zetu kwa mali na hali, ili kuweza kupata umma mwema na bora duniani na akhera.
Mwishoni tunamuomba Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu Wa Ta’ala)Atupe wake, waume na watoto watakaotupa kitulizo cha macho na nyoyo zetu, na Atufanye tuwe viongozi wazuri wa familia zetu. Ewe Mwenyeezi Mungu Mpe Bwana Wetu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Baraka na Amani na Familia yake pamoja pia na Wafuasi wake. “Aamiyn”
No comments:
Post a Comment