Thursday, March 10, 2011

TARATIBU ZA UVAAJI WA MWANADAMU



Muislamu hulichukulia suala la uvaaji kuwa ni miongoni mwa amri za Mola wake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu : "ENYI WANAADAMU! CHUKUENI MAPAMBO YENU (vaeni nguo zenu nzuri) WAKATI WA KILA SWALA; NA KULENI (vizuri) NA KUNYWENI (vizuri). LAKINI MSIPITE KIASI TU. HAKIKA YEYE (Allah) HAWAPENDI WAPITAO KIASI" [7:31]
Mwenyezi Mungu Mtukufu amewapa ruhusa waislamu wale, wanywe na wavae vizuri na pia waende msikitini wakiwa wamevaa nguo nzuri. Na amesema tena : "ENYI WANADAMU! HAKIKA TUMETEREMSHIENI NGUO ZIFICHAZO TUPU ZENU NA NGUO ZA PAMBO; NA NGUO ZA UTAWA (ucha-mungu) NDIZO BORA …" [7:26]
Mwenyezi Mungu anatubainisha kuwa amemteremshia mwanadamu mavazi/nguo za namna mbili :
  1. Vazi la pambo – hili ni kwa ajili ya kuupamba na kuusitiri utupu wake na kumtofautisha na hayawani wengine.
  2. Vazi la ucha-Mungu – hili ni kwa ajili ya kuipamba na kuisitiri nafsi yake na kumfanya binadamu kamili mkamilifu wa utu na ubinadamu. Na hili ndilo vazi bora kama alivyolisifia Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa sababu ni vazi hili ndilo humtoa mwanadamu kutoka kwenye unyama na kumleta kwenye utu.
Mshairi wa kiarabu anaukiri ukweli huu, aliposema :
Ikiwa mtu hakuvaa vazi la ucha-mungu,
Huyo huwa utupu hata kama kavaa,
Na bora ya mambo ya mtu ni kumtii Mola wake,
Hapana kheri kwa mtu mwenye kumuasi Allah.

Na Mwenyezi Mungu anazidi kutuambia : "…NA AMEKUFANYIENI NGUO ZINAZOKUKINGENI NA JOTO ( na baridi, na amekufanyieni) NGUO ZA CHUMA ZINAZOKUKINGENI KATIKA VITA VYENU" [16:81]
Hapa Mwenyezi Mungu Mtukufu anatubainishia aina kuu mbili za mavazi, kulingana na majira ambazo ni :
  1. Mavazi ya joto (kiangazi)
  2. Mavazi ya baridi (masika)
Na pia mavazi maalum ya vita, haya ni pamoja na BULLET PROOF tuzionazo leo. Tunasoma tena : "NA TUKAMFUNDISHA (Daudi) MATENGENEZO YA MAVAZI YA VITA KWA AJILI YENU ILI YAKUHIFADHINI KATIKA MAPIGANO YENU – JE MTAKUWA WANAOSHUKURU ?" [21:80]
Tunafahamikiwa kwamba kumbe sanaa ya utengenezaji wa mavazi ya vita ni sanaa kongwe kabisa na mwanadamu wa kwanza kutengeneza mavazi ya vita ni Nabii Daudi – zimshukie amani-.
Naye mfasiri mkuu wa Qur-ani tukufu, Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – anatufasiria aya hizo kwa kusema : "Kuleni, kunyweni, vaeni na toeni sadaka bila ya israfu (kupita kiasi) wala maringo/fakhri".
Kadhalika, Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – ametufafanulia na kutubainishia mavazi yanayojuzu/yanayofaa kuvaliwa na ambayo ni karaha. Kwa hivyo basi, imempasa na kumlazimu muislamu kuzichunga na kuzifuata adabu/taratibu zifuatazo katika suala zima la uvaaji wake :
  1. Mwanamume asivae kabisa nguo ya hariri kwa hali yeyote ile iwayo hata kama ni tai au kitambaa cha kichwa. Hii ni amri ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – aliposema : "Msivae hariri, kwani atakayeivaa duniani hatoivaa akhera" Bukhaariy na Muslim. Na kauli yake Bwana Mtume il-hali akiwa ameishika hariri kwa mkono na dhahabu mkono wa kushoto : "Hakika (vitu) viwili hivi ni haramu kwa wanamume wa umati wangu" Abu Dawoud.
  2. Nguo yake isiwe ndefu sana kiasi cha kuburuza chini. Urefu wa nguo yake usizidi kifundo cha mguu. Haya yanatokana na kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie - : "Mwenyezi Mungu hatomuangalia/ hatomtazama kwa jicho la rehema atakayeiburuza nguo yake kwa maringo" Bukhariy na Muslim.
  3. Apendelee zaidi kuvaa nguo nyeupe pamoja na kuwa inafaa kuvaa nguo za rangi nyingine. Hivyo ndivyo alivyotuelekeza Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie - : "Vaeni nguo nyeupe kwani hizo ndizo twahara/safi na nzuri sana, na wakafinini maiti wenu kwa nguo nyeupe (yaani washoneeni sanda nyeupe)" Nisaai na Al-Haakim. Na pia imethibiti kwamba Bwana Mtume alivaa nguo ya kijani na alipiga kilemba cheusi.
  4. Mwanamke wa kiislamu avae vazi refu litakaloweza kusitiri hadi nyayo zake, aangushe ushungi kiasi cha kusitiri shingo, na kifua chake. Akifanya hivyo atakuwa ameitii kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isemayo : "EWE MTUME! WAAMBIE WAKE ZAKO NA WANAWAKE WA KIISLAMU WAJITEREMSHIE UZURI NGUO ZAO. KUFANYA HIVYO KUTAPELEKEA UPESI WAJULIKANE (kuwa ni watu wa heshima ili) WASIUDHIWE .." [33:59]Na kauli nyingine isemayo : "…NA WAANGUSHE SHUNGI ZAO MPAKA VIFUANI MWAO NA WASIONYESHE MAPAMBO YAO ILA KWA WAUME ZAOAU BABA ZAO …."
    Na kwa kauli ya Mama Aysha – Allah amuwie radhi- : "Mwenyezi Mungu awarehemu wanawake muhaajirati wa mwanzo, Mwenyezi Mungu alipoteremsha : "…NA WAANGUSHE SHUNGI ZAO MPAKA VIFUANI MWAO …" wakapasua maguo yao mazito na kujitanda nayo" Bukhariy.
    Na kwa kauli ya Ummu Salamah – Allah amuwie radhi - : "Ilipoteremka : "EWE MTUME! WAAMBIE WAKE ZAKO NA WANAWAKE WA KIISLAMU WAJITEREMSHIE UZURI NGUO ZAO …" Walitoka wanawake wa kiansari kama kwamba kuna kunguru vichwani mwao kutokana na maguo waliyovaa na kujitanda" Muslim.
    Hivi ndivyo wanavyotakiwa kuwa waislamu wa kweli, wakiamrishwa pale pale huamrika na wakikatazwa hukatazika pasina kurudi nyuma.
  5. Mwanamume wa kiislamu asivae mavazi na mapambo ya kike na mwanamke muumini asivae mavazi mavazi na mapambo ya kike na mwanamke muumini asivae mavazi na mapambo ya kiume. Anasema Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie - : "Mwenyezi Mungu amemlaani mwanamume anayevaa vazi la mwanamke na mwanamke avaaye vazi la mwanamume kama alivyolaani wanamume wenye kujishabihisha na wanawake na wanawake wenye kujishabihisha na wanamume" Muslim.
  6. Aanze kuvaa upande wa kulia wa nguo yake. Kama ni kanzu, shati, koti, gauni au kizibao aanze kuvaa mkono wa kulia. Kama ni suruali basi aanze kuvaa mguu wa kulia. Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Mama Aysha – Allah amuwie radhi – Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – alikuwa akipenda kuanza kulia katika mambo yake yote; katika uvaaji wake wa viatu, uchanaji wake nywele na kujitwahirisha kwake" Bukhariy.
  7. Aseme anapovaa nguo mpya : Ewe Mwenyezi Mungu wewe ndio mwenye sifa zote uliyenivisha, nakuomba kheri yake na kheri iliyotengenezewa kwayo, na najilinda na shari yake na shari iliyotengenezewa kwayo.
  8. Asivae nguo nyepesi yenye kuonesha ndani rangi ya mwili wake (transparent). Kadhalika asivae nguo yenye kumbana sana kiasi cha kuchora ramani/finyango la mwili wake.

Tuesday, March 8, 2011

Fiqh Ya Kuwaita Majina Watoto


Fiqh Ya Kuwaita Majina Watoto

Kutoka kwa "Al-Minhaaj Al-Qawiym `ala al-Muqaddimah al-Hadhwramiyyah"
Imefasiriwa na Iliyaasa Maulaana



Ni Sunnah kutunza jina zuri, na katika majina mazuri ni 'Abdullaah (Mtumwa wa Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Ta'aala) na 'Abdur-Rahmaan (Mtumwa wa Mwingi wa Rehema); na majina ya ki kweli hasa ni Al- Haarith (Anayezaa) na Humaam (Hodari); na majina mabaya zaidi ni Harb (Vita) na Murrah (Chungu) Hadiyth ifuatayo imethibitisha,
((Majina yanayopendezewa kwa Allaah (Subhaana wa Ta'aala)   ni 'Abdullaah na Abdur-Rahmaan.))  [imeripotiwa na Muslim. Kwa Abu Daawuud kuna nyongeza ((Na majina ya ki kweli hasa ni al-Haarith na Humaam, na mabaya zaidi ni Harb na Murrah)).
Na majina mabaya, na yale ambayo yanamaanisha  vitu vibaya katika kutokuwepo kwao, ni makuruhu (Yasiyopendeza), kama vile Nujayh (fanikiwa), Barakah (baraka), Kulayb (kijimbwa), Harb (vita), Murrah (chungu), Shihaab (kimondo), Himaar (punda), Aflah (fanikiwa sana), Yasaar (wepesi), Rabaah (faida), na Naafi` (kunufaika) na majina kama Sittun-nisaa (mwanamke wa wanawake wote)  ni yanayogombezewa sana.  Na Mfalme wa Wafalme limekatazwa, kama ilivyokuwa 'Shahenshaah', na Aqdhaal-Qudhaat (hakimu wa mahakimu).
Na inapendelewa kubadilisha majina mabaya na ambayo yanamaanisha vitu vibaya katika kutokuwepo kwao. Na inapendelewa kwa mtoto wa kiume, mwanafunzi au mfanyakazi kutomwita kwa jina lake, na kwamba watu wazuri (wanaume na wanawake) wawe wana kun-yah, hata ikiwa hawana watoto wa kiume, na kun-yah huhusiana na mtoto wa kiume wa mwanzo; na imekatazwa (Haraam) kuwa na Kun-yah ya 'Abul-Qaasim kwa mtu ambaye jina lake ni Muhammad na vile vile kwa watu wengine, katika kipindi cha Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na vile vile baadae ya hapo. Tanbihi (imewekwa): Kuna khitilafu baina ya madhehebu juu ya mawazo katika nukta hii- wengine wameshika kwamba katazo lake liliwekwa katika kipindi cha Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).     
Na aliyeruka mipaka (faasiq) au mzushi asipewe kun-yah mpaka kukiwepo hofu ya fitnah, au ikiwa kwa sababu ya utambulishi, (kama vile Abu Lahab). Na inapendelewa kwamba mtu asitumie kun-yah yake pekee (yaani bila ya kutimiza jina lake pia), isipokuwa akiwa anajulikana kwa kun-yah yake na sio kwa jina lolote isipokuwa hilo. Na pia imekatazwa (Haraam) kumtania mtu kwa jina ambalo halipendi. Kama ikiwa anajulikana kwa jina jengine (ambalo halimchukizi) na hata kama jina hilo lina dhamiria kitu ambacho kinamhusu yeye ambacho ni cha kweli.

Kun-yah (Lakabu au Jina la kupachika)
Ushahidi uliombwa wa kuchukuliwa kun-yah kuwa ni Sunnah. Kuna vidokezo mbali mbali juu ya hili katika Hadiyth. Ya kwanza, Mtume  (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na kun-yah, na hakuna ushahidi wowote wa kuonyesha kwamba kuwa na kun-yah ilikuwa kwa yeye pekee, na hii ndio inayoamua ni Sunnah (kumfuata mtu katika kitu ambacho hakikua kwa ajili yake pekee (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na kuna Hadiyth ya kuwaita watu kwa jina la Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) (Muhammad) lakini si kwa kun-yah yake (Abul-Qaasim), ambayo kwa mara nyingine  bila shaka inaamuliwa tuwaite watu pamoja na kun-yah. Zaidi, kuna Hadiyth iliyoripotiwa na At-Tirmidhiy  "al-Shama'il Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwita mvulana mdogo kwa kun-yah, kuonyesha kwamba si muhimu kuwa na mtoto kabla ya kutumia kun-yah. Mazungumzo zaidi ya Hadiyth hizi yanapatikana katika Fat-h al-Baariy (maelezo ya Sahiyh al-Bukhaariy).

»

Manufaa na Matatizo ya Ndoa


Imefasiriwa na Ummu Ahmad

 

MANUFAA YA NDOA
1. Kupata kizazi ambacho kwanza kitasaidia katika ujengaji wa jamii, pili kueneza jinsia ya watu wa kila kabila au mataifa mbali mbali, na kubwa zaidi ni kuongeza idadi ya kizazi cha jamii ya kiislamu.
2. Kumridhisha Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa   kueneza idadi ya wafuasi wa dini ya Kiislamu.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika hadithi sahihi:
“Oeni wake wema muwapendao na wataowapatia kizazi chema, kwani siku ya Kiyama nitajivunia ukubwa wa umati wangu.” [Imam Ahmad]
   3. Kupata baraka za mtoto mwema ambaye atakayemsomea dua mzee wake (atakapofariki). Maneno haya yamethibitishwa na hadithi maarufu inayosema kuwa:
“Binaadamu anapokufa, basi amali zake nzuri hukatika au humalizika, isipokuwa mambo matatu makuu nayo ni: Sadaka yenye kuendelea, Elimu yenye kunufaisha na Mtoto mwema atakayemuombea dua mzee/wazee wake.” [Riyadhus-Swaalihiyn]
Faida nyenginezo zipatikanazo katika ndoa ni:
4.    Kinga kutokana na shetani katika mambo yanayopelekea au yanokaribisha tendo la zinaa.
5.    Utulivu wa akili na moyo na kuwa na urafiki ambao hupelekea mapenzi na huruma baina ya mume na mke.
6.    Kunganisha kwa Familia za pande mbili za uukeni na uumeni.
7.   Kusaidiana katika kazi za nyumba (sio kumuachia mke kazi zote za ndani ya nyumba). Hii ni tabia ambayo ingalipo kwa baadhi ya akina baba. Kwa vile tabia hii imekuzwa na utamuduni wetu wa tunakotoka, kinyume kabisa na maamrisho ya dini yetu ya kiislamu yanavyotuagiza.
8.   Kuelimishana majukumu ya kifamilia. Pia kuweka bidii na kuwa tayari   kuihami na kuitunza familia. Na vile vile kuishughulikia na kuitimizia mahitaji yake yakiwa ama ya (kimwili, kimavazi, kisiha, kimawazo na kiroho) na kustahamiliana pale panapotokea kutoelewana.
MATATIZO KATIKA NDOA
Wakati huo huo kuna matatizo yanayopatikana katika ndoa ambayo inabidi tuzingatie na kujichunga ili tuepukane na matatizo hayo. Nayo ni kama yafuatayo:
1.     Kushindwa kuchuma pato la halali, ambapo itapelekea kutafuta njia ambazo si za halali za kimapato ili kuweza kutimiza mahitaji ya familia. Haimfalii mke kumlazimisha mumewe ampatie mambo yaliyo nje ya uwezo wa mume. Na tuwaige wanawake wema waliopita, ambao kila waume zao wakitoka kwenda kwenye shughuli zao za kutafuta riziki, wakiwausia kuwa wasirejee na chochote cha haramu. Wakiwanasihi waume zao kuwa ni bora wastahamili kwa njaa ya hapa duniani kwani adhabu ya kesho akhera sio ya kustahamilika.
2.      Kushindwa kutimiza majukumu ya ndoa, na hasa kutimiza haki za mke au kutoweza kustahamili kwenye wakati mgumu wa kimaisha. Na tuwe makini katika suala hili kwani kuna ile dhana ya kuwa ndoa ni jambo la kujionyesha tu kuwa fulani kaoa au kaolewa.
“Kila mmoja kati yenu ni mchungaji, na kila mmoja kati yenu atapaswa kuulizwa ya juu ya kile anachokichunga. Mume ni mchungaji wa familia yake, naye atapaswa kuulizwa juu ya anaowachunga. Na mke ni mchungaji wa nyumba ya mumewe, naye pia atapaswa kuulizwa juu ya anachokichunga. Hivyo basi, kila mmoja kati yenu ni mchungaji ambaye atapaswa kuulizwa juu ya anaowachunga” (Bukhari, Muslim)
     3.      Kuacha kushughulikia mambo muhimu ya kidini, kwa mfano kutumia muda mwingi katika mambo ya anasa za kidunia kama vile kuangalia Televisheni, kwenda kwenye shehere za kuzaliwa mtoto au kwa kutimiza umri fulani wa mtoto (birthday na party), badala ya kutumia muda huo kwa kutengeneza maisha ya akhera ambayo ndio ya milele. Kama tunavyotanabahishwa kwenye Quraan Tukufu  Sura ya sitini na tatu aya ya tisa.
((Enyi mlioamini! Yasikusahaulisheni mali yenu, wala watoto wenu, kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Na wenye kufanya hayo ndio walio katika khasara))
[Al-Munaafiquun:63:9]
Mtunzi wa mada hii amemalizia kwa kusema kuwa:
Dinar unayoitumia katika njia za Mwenyeezi Mungu  (Subhaanahu Wa Ta'ala), Dinar unayoitumia kumuachia huru mtumwa, Dinar unayoitumia katika kutoa sadaka kwa mtu anayehitaji sadaka hiyo, basi hakuna Dinar iliyo bora kati ya dinar hizo ila ile unayoitumia kwa ajili ya familia yako.
Msemo huu una maana ya kwamba hakuna jambo muhimu katika mafundisho ya kijamii ya kiislamu kama lile la kuzishughulikia familia zetu kwa mali na hali, ili kuweza kupata umma mwema na bora duniani na akhera.
Mwishoni tunamuomba Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu Wa Ta’ala)Atupe wake, waume na watoto watakaotupa kitulizo cha macho na nyoyo zetu, na Atufanye tuwe viongozi wazuri wa familia zetu. Ewe Mwenyeezi Mungu Mpe Bwana Wetu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Baraka na Amani na Familia yake pamoja pia na Wafuasi wake. “Aamiyn”

FADHILA ZA HIJAB

 
Imefasiriwa na Salwa Muhammad Mbaaruk


Hijaab ni tendo tiifu kwa Allaah na kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kasema katika Qur-aan;

{{Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanapokata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi.}} Al-Ahzaab: 36

Mwenyeezi Mungu (Subhaanahu wa Ta‘ala) pia kasema;

{{Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao (juyuubihinna) juu ya vifua vyao}} An-Nuur: 31

Juyuubihinna: Wanachuoni wastahifu kutoka katika zama za as-Salafus Swaalih (watangu wema) wamekhitalifiana kama vazi (Jilbaab) linalofunika mwili lazima lifunike mikono na uso au laa. Leo, wanachuoni wanaoaminika wanasema kuwa mikono na uso lazima ifunikwe. Wanachuoni wengine wanasema bora kwa wanawake kufunika mwili wao mzima.


Hijaab ni ‘Iffah (Stara)
Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kaifanya Hijaab dhahiri kuwa ni takaso na hayaa. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kasema:

{{Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu}} Al-Ahzaab: 59


Katika aya hiyo hapo juu kuna ushahidi kuwa utambulifu wa kuonekana uzuri wa mwanamke ni madhara kwake. Na pindi sababu hiyo ya vile vyenye kusababisha mvuto na vishawishi vitakapoondoka, basi makatazo hayo huondoka. Hii ni kama tunavyoona kwa upande wa wanawake vizee ambao wanaweza kuwa wamepoteza kila kipengele cha kuvutia. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kahalalisha kwa wao kuweka pembeni buraa zao na kuonyesha sura na mikono yao, lakini ni bora zaidi kuweka stara zao.


Hijaab ni Twahara (Utakaso)
Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kautonyesha hekima nyuma ya Sheria ya Hijaab:

{{Na mnapowauliza wakeze haja waulizeni nyuma ya mapazia. Hivyo ndio usafi zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao.}} Al-Ahzaab: 53

Hijaab ni muundo wa usafi kwa mioyo ya waumini wa kiume na kike kwa sababu ni kinga au kiziuzi dhidi ya matamanio ya moyo. Bila ya Hijaab, moyo unaweza kutamani mambo machafu. Na hivyo ndio maana moyo upo safi zaidi wakati mwanamke anapojifunika, au kuhifadhiwa (na Hijaab) na vile vile inazuia fitna (matendo maovu). Hijaab inakata taamuli (fikra) mbovu na matamanio mabovu ya moyo.

{{Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine. Kama mnamcha Mungu basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake. Na semeni maneno mema.}} Al-Ahzaab: 32


Hijaab Ni Ngao

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:

Allaah, Aliye juu, ni Pepo, ni Hayii (Mwenye Kustahi), Sittiyr (Kinga). Anapenda Hayaa na Sitr (Kinga)” (Abu Daawuud)


Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia kasema:

((Mwanamke yeyote anayevua (hajisitiri sawasawa) nguo zake mbele ya yeyote zaidi ya mume wake (ima kwa kuijionyesha au kusifiwa), amevunja kinga ya Mwenyeezi Mungu juu yake)).


Hadiyth hii inaonyesha namna ambavyo kitendo kinalipwa kutokana na uzuri au ubaya wake.


Hijaab ni Taqwah (Ucha Mungu)

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:


{{Enyi wanaadamu! Tumekuteremshieni nguo za kuficha tupu zenu, na nguo za pambo. Na nguo za ucha Mungu ndio bora. Hayo ni katika Ishara za Mwenyezi Mungu mpate kukumbuka}} Al-A‘araaf:26


Hizi zama tulizonazo hivi sasa, mtindo mingi ya mavazi iliyopo ulimwenguni leo, ni ya kujionyesha tu na aghlabu sana kuchukuliwa kama ni stara ya mwili wa mwanamke. Lakini kwa wanawake waumini, makusudio ni kujihifadhi miili yao na kuficha maumbo yao. Kama walivyoamrishwa na mwenyewe (Allaah). Na hilo ni tendo la Taqwa (Ucha Mungu).


Hijaab Ni Iymaan


Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Hakuyaeleza maneno yake kuhusu Hijaab ila kwa wanawake Waumini (al-Muuminaat). Katika sehemu nyingi kwenye Qur-aan Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anarejea kutaja "Wanawake Waumini"! Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha), mke wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), aliwambia baadhi ya wanawake wa kabila la Banu Tamiym waliokuja kumtembelea yeye (Radhiya Allaahu ‘anha) na wakawa wamevaa nguo nyepesi, yaani nguo ambazo si stara kwa mwanamke wa Kiislam. Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akawaambia: “Ikiwa nyinyi ni wanawake Waumini, basi hakika, hilo sio vazi la mwanamke Muuminah analotakiwa kuvaa, na ikiwa sio wanawake Waumini, basi shauri yenu ikiwa mnaona mnafaidika


Hijaab ni Hayaa


Kuna Hadiyth mbili Sahihi ambazo zinasema: “Kila Dini ina maadili na maadili ya Uislamu ni Hayaa” (Ibn ‘Abdil-Barr, al-Mundhiry na kutoka katika kitabu cha at-Targhiyb wa at-Tarhiyb cha Shaykh al-Albaaniy), na “Hayaa ni katika Iymaan na Iymaan imo katika Pepo” (at-Tirmidhy)


Hijaab ni (Ghiyrah) Ghera


Hijaab inaungana na hisia za kimaumbile ya Ghera, ambayo ni lazma kwa mwanamme aliyekuwa hapendi kuona watu wakimwangalia mke na watoto wake wa kike. Ghera ni mtukutiko unaochemka kwa mwanamme unaomsukuma kuona wivu na kuwakinga wanawake waliokuwa wamehusiana nae kutoka kwa wageni na wasio Maharimu zao. Mwanamme mkamilifu wa Kiislamu ana Ghera (wivu) kwa wanawake wote wa Kiislamu kuwakinga hao wanawake na matamanio na uchu wa wanaume. Katika Itikio la matamanio, wanaume wanawaangalia wanawake wengine kwa uchu na matamanio na hawajali kama wanaume wengine wanafanya hayo kwa wake zao na watoto wao wa kike. Mchanganyiko wa kijinsia na kukosekana Hijaab ni jambo lenye kuangamiza Ghera ya wanaume. Uislamu unachukulia Ghera ni sehemu ya Iymaan. Heshima ya mke na binti au mwanamke yeyote wa Kiislamu ni lazima iheshimiwe na kulindwa.